Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
KOROGWE WAANDIKISHA BIMA ZA AFYA 1000
10 Oct, 2024
KOROGWE WAANDIKISHA BIMA ZA AFYA 1000

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki katika Uzinduzi wa Zoezi la Uandikishaji wa Bima za Mufti elfu moja (1000) katika Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga zoezi ambalo pia limehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Baraza Kuu ya la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wakiongozwa na Naibu Mufti, Sheikh Ally Ngeruko ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. William Mwakilema.

Tukio hilo ni muendelezo wa programu ya ugawaji wa Bima za Afya elfu kumi alizoahidiwa na  Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuberi akishirikiana na Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware ambapo mpaka sasa watanzania zaidi ya elfu tatu wameshafikiwa na bima hizo na baadhi yao wameshaanza kunufaika nazo.

Kupitia zoezi hili Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ilipata fursa ya kutoa elimu ya bima kwa wanakorogwe wakiwakilishwa na Bw. Ayubu Mremi, Afisa Takwimu Bima na Bw. Abubakari W Kafumba, Afisa Uhusiano kwa Umma wakiwafikia watu mbalimbali waliojitokeza katika zoezi la kujiandikisha ili kupata bima hizo za mufti.

Bima hizo zitatolewa kwa watu 100 kila kata hasa wenye uhitaji wakiwemo wajane, wagane, watoto wanaoishi katika mazingira magumu, yatima, watu wenye ulemavu na watu wasio na uwezo bila kujali dini wala kabila ili kuepuka changamoto ya kukosa matibabu kutokana na hali ngumu ya kifedha au kukosa pesa ya matibabu na hatimaye kufikia lengo la bima elfu moja zilizokusudiwa kutolewa Korogwe. 

“Hii ni hatua ya mafanikio hivyo ujio wa Bima ya mufti kwa kushirikiana na TIRA utaleta mwamko kwa viongozi katika jamii zao na kuwa chachu ya kuleta mabadiliko na suluhu ya changamoto za masuala ya kiafya na pia kwa umuhimu hii ni hatua kubwa ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya bila kikwazo”. Amesema Sheikh Ally

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. William Mwakilema ameeleza kuwa Serikali iko mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Mufti na TIRA kwani ndio mfano wa uongozi bora wenye kuwajali wananchi wake ukiakisi jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwafikia na kuwagusa watanzania wote.