Mkutano wa kupokea na kusikiliza malalamiko ya Bima uliofanyika kanda ya kati - Dodoma .
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) tarehe 27.04.2023 iliandaa mkutano wa kupokea na kusikiliza malalamiko ya Bima uliofanyika kanda ya kati - Dodoma katika ukumbi wa Morena Hoteli.
Pichani waliokaa ni Mwenyekiti wa Mkutano huo na pia Balozi wa bima nchini Mhandisi. Zena Said (Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Zaznibar) katikati, Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo A. Sagware wa tatu kulia, Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija I. Said wa tatu kushoto, Meneja wa Kanda ya Kati wa TIRA Bw. Shaarif Hamad wa kwanza kulia, Mwakilishi wa Makampuni ya Bima Bi. Merina Hussein wa kwanza kushoto, Mhe. Wanu Hafidh Mbunge wa Jamhuri na Balozi wa Bima nchini wa pili kulia na Mhe. Josephat Hassunga Mbunge wa Jamhuri na Balozi wa Bima nchini wa pili kushoto. Waliosimama ni Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Mkutano huo umefanyika ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya Bima nchini ambapo Mamlaka imekuwa ikifanya kwa lengo la kupokea na kutatua changamoto mbalimbali wanazozipata wadau watumiaji wa bima nchini, kupata maoni na ushauri ya wadau watumiaji wa bima, watoa huduma za bima na wananchi wanufaika wa bima.
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware, aliwaeleza washiriki kwamba ni muhimu kujadiliana na kushirikiana katika kukuza soko la Bima. Aidha ni matarajio ya TIRA kuendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi watumiaji wa bima na malalamiko ya kisera mamlaka itaendelea kuishauri serikali. Pia alitoa rai kwa watoa huduma za bima kushughulikia malalamiko ya wananchi watumiaji wa bima kulingana na sheria, kanuni na kwa kufuata miongozo mbalimbali inayotolewa na Mamlaka. Mwisho kabisa, alisisitiza kuwa TIRA ipo tayari kuendelea kupokea na kuyashughulikia malalamiko, maoni na ushauri wa wadau wa Bima kwa lengo la kukuza na kuendeleza sekta ya bima nchini.
Aidha, Mhe. Josephat Hassunga Mbunge wa Jamhuri na Balozi wa Bima alitoa maelekezo kwa washiriki na wananchi kutumia huduma za bima ili kujikinga na majanga na maafa mbalimbali yanapotokea. Pia alisisitiza kuwa ni muhimu kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya Bima kwa wananchi hasa vijijini ili kukuza sekta ya bima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Balozi wa bima nchini Mhandisi. Zena Said (Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar) alisisitiza kuwa ni muhimu kwa Taasisi za Serikali kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kukuza pato la Taifa kwa ujumla. Aidha alielekeza Mamlaka (TIRA) kuendelea kusimamia haki za watumiaji na watoa huduma za bima kulingana na sheria, kanuni na miongozo mbalimbali, pia kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi hasa vijijini. Mwisho kabisa, aliipongeza TIRA kwa juhudi mbalimbali zinazofanyika katika kukuza na kuendeleza soko la bima ikiwemo kuandaa mikutano ya namna hii.