Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
NJOMBE: KAMISHNA WA BIMA ASISITIZA UMUHIMU WA BIMA YA AFYA KWA WOTE , MKOA KWA MKOA KUTOA UELEWA WA BIMA
07 Aug, 2024
NJOMBE: KAMISHNA WA BIMA ASISITIZA UMUHIMU WA BIMA YA AFYA KWA WOTE , MKOA KWA MKOA KUTOA UELEWA WA BIMA

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Ofisi ya Kamishna wa Bima na ujumbe wake wamemtembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe leo Agosti 7, 2024 ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kuwatembelea Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika Kanda ya Juu kusini inayojumuisha Mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Ujumbe huo ukiongozwa na Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware umekutana na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe wakiongozwa na Kaimu Katibu Tawala Njombe, Bw. Edward Mwakipesile ambapo lengo kuu la ziara hii ni kutoa elimu ya bima kwa wakuu wa mikoa na wilaya ili waweze kuhimiza matumizi ya bidhaa na huduma za bima katika jamii zao na hatimaye kuweka misingi ya ushirikiano na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kulinda haki za watumiaji wa bima na kuhakikisha huduma za bima zinawafikia wananchi kwa urahisi na uwazi.

Aidha, Dkt. Saqware ameeleza kuhusu umuhimu na hatua za utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kuwahimiza wananchi hususan wananjombe na hatimaye wawe watumiaji wa bima hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu, sekta ndogo ya Bima imeendelea vizuri kila mwaka ambapo watoa huduma za Bima wanaongezeka kwa zaidi ya asilimia 10% hadi kufikia watoa huduma 1,610 mwaka 2023. Aidha, watumiaji wa bidhaa na huduma za Bima wameongezeka kutoka milioni 6 mwaka 2022 hadi kufikia milioni 12 mwaka 2023 sawa na asilimia 20 ya wananchi, amesema Dkt. Saqware.

Kwa muktadha huu Kamishna wa Bima pia amesema kuwa ili kufikia ukuaji wa Sekta ndogo ya bima kwa angalau asilimia 15 katika miaka 5 ijayo, Mamlaka imeainisha vipaumbele kadhaa ikiwemo ukamilishaji wa Sera ya Bima ya Taifa na mkakati wake wa utekelezaji, ukamilishaji wa Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote na Miongozo husika ya usimamizi, ukamilishaji wa Kanuni za Bima za Lazima, ukamilishaji wa Kanuni za Bima za Kilimo, uanzishaji na utekelezaji wa Skimu ya Taifa ya Bima za Kilimo, ukamilishaji wa utaratibu wa kisheria wa uanzishwaji wa Bodi ya Wataalam wa tasnia ya Bima, Hifadhi ya Jamii na Utathminishaji (ISPAB).

Kupitia tukio hili Mamlaka imeiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iwahamasishe wakuu wa wilaya, Makatibu tawala na wananchi wa mkoa wa Njombe kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na kutoa ushirikiano katika kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananjombe na kujenga uelewa wa bima ili wabaini manufaa ya kutumia bima kama kinga mahsusi kwa maisha, afya na mali zao.

wa upekee mkubwa Kamisha wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware ametumia fursa hii pia kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka kuwa Balozi wa TIRA katika utoaji wa elimu ya bima kwa wananjombe, kuwahamasisha kutumia bidhaa na huduma za bima, hususan bima za afya na kilimo.
 
Sambamba na hilo, Kamishna amemtabulisha Meneja wa Kanda ya Juu Kusini Bi. Neema Lituli ambaye atahakikisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe inapatiwa ushauri wowote wa kitaalamu kuhusu bima akishirikiana na Kampuni za bima zilizopo kwenye Kanda ya Juu Kusini.
 
Kupitia ofisi za kanda, Mamlaka itaendelea kuhakikisha soko la bima la Tanzania linaendela kuwa himilivu, lisilo na udanganyifu, lenye weledi na lenye tija.