Katibu mkuu Kiongozi awapokea Mabalozi wa Bima
Leo tarehe 1 Septemba, 2023 Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Mhandisi ZENA A. Saidi wamefanya kikao cha siku moja na Viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ambapo ametambulishwa rasmi na kuwapokea Mabalozi wa Bima na pia kujadili maendeleo ya sekta ya bima nchini.
Mabalozi wa Bima waliotambulishwa katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar ni Mhandisi Zena A. Said Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Japhet N. Hasunga Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mhe. Wanu H. Ameir Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Mabalozi hao walioteuliwa Mwezi Februari 2023 majukumu yao ni Kutoa ushauri kwa Mamlaka na sekta ya bima kwa ujumla kuhusu maendeleo ya sekta ya bima na pia kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya bima katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi na Makatibu Wakuu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Balozi Dkt. Kusiluka pamoja na kukubali kuwa Balozi wa vitendo wa bima, amesema Makampuni ya bima yaongeze wigo wa bidhaa zao za bima na pia Mamlaka iendelee kutoa elimu kuhusu vipengele mbalimbali vya bima ambazo Serikali, mashirika binafsi na mtu mmojammoja wanaweza kuzitumia. Amesema Serikali ina mpango wa kupanua wigo wa kuzikatia bima mali zake mbalimbali baada ya utafiti kufanyika juu ya aina na gharama za kukatia bima mali hizo.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Dkt. Juma M. Akili Katibu Mkuu ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar pamoja na Dkt. Natu E. Mwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni watendaji wakuu katika wizara Mama ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Katika maelezo yake ya Utangulizi Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Mhandisi Zena A. Saidi amesema tangu kuchaguliwa kwa mabalozi Mwezi Februari 2023 tayari wamepata mafunzo kuhusu umuhimu wa bima ambapo imewajengea uwezo wa kutoa elimu kwa umma na kwa wabunge. Mabalozi wamekuwa mstari wa mbele kuishauri Serikali kuhusu umuhimu wa ukatiaji bima wa mali za Serikali.
Akielezea mafanikio katika sekta ya bima Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware amesema Mchango wa Sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56% kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68% kwa mwaka 2021. Pia Mamlaka imeendelea kuongeza gawio Serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 Mamlaka imeweza kulipa gawio kwa Serikali la jumla ya Tsh. Bilioni 2.9.
Kwa upande wa ajira Kamishna amesema sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173 ukilinganisha na 3,208 kipindi kama hicho mwaka 2021.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa azimio la kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kuendelea kutoa elimu kwa watu mbalimbali wakiwemo Makatibu Wakuu na Wabunge. Imeelekezwa semina ya Bima ifanyike kwa Makatibu Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Makatibu wa Serikali ya Mapandizi ya Zanzibar.
Upande wa TIRA pia uliwakilishwa na Naibu Kamishna Bi Khadija Said, Meneja Ubora na Udhibiti wa Vihatarishi Bw. Zakaria Muyengi pamoja na Meneja Uhusiano na Mawasiliano Bi. Hadija Maulid.