Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote yachochea upatikanaji wa huduma za matibabu nchini
Kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kutaongeza mchango wa sekta ya bima katika kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya. Hayo yalibainishwa wakati Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, alipozindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) tarehe 21 Januari 2025, jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Jenista Mhagama alisema:"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amemaliza kazi yake ya kuwekeza katika huduma za matibabu. Sasa kazi yenu ni kuhakikisha wananchi wanatumia huduma hizo kupitia bima ya afya. Ni matarajio yangu kuwa bodi hii mtasimamia jukumu hili kwa nguvu zote."
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, aliyehudhuria uzinduzi huo, alieleza jinsi sekta ya bima imechukua hatua katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za matibabu kupitia mifumo ya bima.
Aidha, sekta ya bima nchini imeendelea kuimarika kwa kasi, ambapo mchango wake katika pato la taifa umefikia asilimia 2.01 kufikia mwaka 2023. Wanufaika wa huduma za bima, wakiwemo wale wa bima ya afya, wameongezeka hadi kufikia milioni 23, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 29 kwa mwaka ukilinganisha na miaka ya nyuma. Pia, idadi ya watoa huduma wa bima imeongezeka kwa asilimia 24 kufikia mwaka 2024.
Kwa muktadha huu, ni dhahiri kuwa sekta ya bima iko mstari wa mbele katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa watoa huduma wa bima ya afya wanawafikia Watanzania wote, na hivyo kuchochea upatikanaji wa matibabu bila vikwazo vya kifedha.