Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Siku ya Bima yang’ara Zanzibar
15 Sep, 2023
Siku ya Bima yang’ara Zanzibar

Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) wamefanya kongamano kubwa la Siku ya Bima Nchini katika Hoteli ya Verde Zanzibar 15 September 2023 huku Mgeni Rasmi  akiwa Mh. Hemed Suleiman Abdulal, Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akimwakilisha Mh. Dkt. Hussein Ally Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mkt. wa Baraza la Mapinduzi.

 Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa chama na Serikali, wakiwemo Katibu mkuu kiongozi na katibu wa baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said, Mh. Japhet Hasunga, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao pia ni Mabalozi wa Bima.

Akiwakaribisha wageni, Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) Bi. Magreth Ikongo, alieleza mchakato mzima wa Maandalizi ya Kongamano hilo ambalo lilianza kwa kufanya matendo ya Huruma ikiwemo kwenda kutoa vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Mwananyamala Jijini Dar es salaam, lakini pia wamefanikiwa kutoa Kompyuta 10 katika shule ya Sekondari Mikindani iliyopo Dole Mjini Zanzibar, Matembezi ya Bima yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Naye Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware alieleza mipango mbalimbali ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kushirikiana na Serikali kama vile, Kuandaa Skimu ya bima ya Kilimo, Bima ya Afya kwa wote, Mpango wa kukatia Bima vyombo vya Serikali, kutoa miongozo mbalimbali inayosimamia haki ya mkatabima.

Wakati wa Hotuba yake, Mgeni Rasmi, Mh. Hemed Suleiman Abdullah, Makamu wa Rais wa pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, aliipongeza Sekta ya bima kwa kuwa na Mchango mkubwa katika kuongeza pato la serikali lakini pia aliipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kushirikiana na Taasisis nyingine kama vile UDSM, PSSSF, IFM, SUZA, IFM na Taasisi nyingine kwa kuanza mchakato wa kuanzisha Bodi ya Wataalam wa Bima Hifadhi ya jamii na Watakwimu bima (Insurance Social protection and Acturial Board). Vile vile alikubaliana na Ombi la Naibu Kamishna wa Bima la kutaka magari yote yanapopata leseni, yakatiwe bima kabla hayajaingia Barabarani, hii itasaidia kwa baadhi ya wamiliki wa magari kukwepa Bima.

Kongamano la Siku ya Bima huadhimishwa kila mwaka ambapo huu ni mwaka wa 26.