Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshirikiana na Benki ya NMB kutoa mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya dhamana
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshirikiana na Benki ya NMB kutoa mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya dhamana (Trust Account) kwa kampuni za bima nchini katika ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Semina ilifunguliwa na Mgeni rasmi Mh. Mudrik Ramadhan Soraga Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezeji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akifungua semina hiyo, Mh. Mudrik Ramadhan Soraga ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) pamoja na benki ya NMB kwa kuanzisha Akaunti ya Dhamana ya Bima (Trust Account).
Mh. Soraga amesema uanzishwaji wa Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kuendana na matakwa ya kisheria na udhibiti yaliyowekwa na TIRA.
Vile vile, amesema utaratibu uliokuwa ukitumika mwanzoni katika usimamizi wa dhamana ya bima haukuwa mzuri jambo ambalo lilipelekea TIRA kushindwa kusimamia vizuri amana hizo pindi ziliporejeshwa kwa makampuni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) baada ya kuiva.
Amesema kuwa kampuni nyingi za bima zilikuwa zikitumia fedha za amana ya Akiba katika matumizi mengine, pasipo kupata idhini ya TIRA hivyo kupelekea kuingia katika changamoto ya ukwasi, na wakati mwingine kushindwa kulipa fidia kwa wateja kutokana na fedha kuwekezwa katika miradi mingine.
Aidha, alibainisha kuwa uamuzi wa kufungua Akaunti ya Dhamana ya Bima katika benki za biashara ni mwarobaini wa changamoto hiyo, kwani sasa TIRA itaweza kusimamia moja kwa moja fedha hizo za amana za akiba, jambo ambalo si tu litaimarisha usimamizi, bali pia litaboresha maendeleo ya sekta ya bima nchini.
Akizungumza katika semina hiyo, Kamishina wa Mamlaka ya Bima Nchini, Dkt. Baghayo A. Saqware amesema chimbuko la Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 inayozitaka Kampuni za Bima kuweka Amana za Usalama angalau 50% ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima.
Dkt. Saqware amesema mwaka jana Mamlaka kwa kushirikiana na Chama cha Makampuni ya Bima Tanzania (ATI), walikubaliana kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji wa Usimamizi wa Ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.