Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya mkutano wa nne
15 May, 2023
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya mkutano wa nne

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya bima, hifadhi ya jamii, na wataalam wa Takwimu Bima imefanya mkutano wa nne kujadili uanzishwaji wa bodi ya kitaalama ya Bima, Hifadhi ya Jamii, na Watakwimu Bima (ISPAB).

Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu akiwa mgeni rasmi. Prof. Katundu alishukuru jitihada za Mamlaka za kuongoza katika mchakato wa awali wa kuanzisha bodi hii muhimu ya kitaaluma.

"Lazima tuchukue hatua haraka ili kuwa na bodi kitaluuma ambayo itasimamia haki na maslahi  ya wataalam wa Bima, Ulinzi wa Jamii, na watakwimu kwani kulingana na takwimu zilizopo kada hizi tatu zina zaidi ya watalaamu elfu nne lakini hawana bodi inayokagua mienendo yao ya kila siku ya kiutendaji,” alisema Prof. Katundu.

Kwa upande mwake, Kamishna wa Bima, Dk.Baghayo Saqware aliwasisitiza washiriki tambua kuwa ni jukumu la wadau wote kuhakikisha bodi hiyo (ISPAB) inaanzishwa kwa manufaa ya wataalam wote wa bima na hifadhi ya jamii ili kuhakikisha wateja wanaowahudumia wanapata haki zao kwa mujibu wa miongozi ya kitaaluma.

Wadau walikubaliana kuundwa kwa timu kutoka taasisi shiriki ili kuweza kuandaa taarifa mbalimbali zitakazorahisisha upatikanaji wa bodi ya ISPAB. Mkutano huo ulifanyika ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya kujadili uanzishwaji wa Bodi ya Bima, Hifadhi ya Jamii, na Takwimu Bima (ISPAB) ikiwa na ajenda za kuwasilisha pendekezo la uanzishwaji wa ISPAB, uwasilishaji wa Hadidu za Rejea (ToRs) kwa ajili ya kuajiri Mshauri Mwelekezi, na uwasilishaji wa bajeti.