Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Mkutano Mkuu Wa Mawakala wa Bima Nchini kupitia Umoja wao (IAAT)
28 Jun, 2023
Mkutano Mkuu Wa Mawakala wa Bima Nchini kupitia Umoja wao (IAAT)

Tarehe 26.06.2023 Mawakala wa Bima Nchini kupitia Umoja wao (IAAT) chini ya uongozi wa Mwenyekiti Bw. Sayi John Daudi walifanya Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam. Lengo la Mkutano huo ilikuwa ni kujadili mambo mbalimbali yanayolenga kuendeleza na Kuimarisha soko la Bima. Hata hivyo, wakati wa mkutano huo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na Miongozo iliyotolewa na Mamlaka, Utekelezaji wa Mabango ya Wakala wa Bima “Standard Singnboards”, na Marekebisho ya Sheria ya Bima kupitia Sheria ya Fedha Na. 05 ya mwaka 2022.

Aidha katika Mkutano huo Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware alishiriki kama Mgeni Rasmi akiambatana na baadhi ya wafanyakazi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA). Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawakala wa Bima mbalimbali kutoka mikoa ya Mwanza, Mbeya, Mtwara, Arusha, Pwani, Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam na mikoa mingine.

Katika hotuba yake Kamishna wa Bima aliwasisitiza washiriki kusikiliza mada zitakazotolewa kwa kuwa ni mada zilizo stahimilivu katika kukuza sekta ya Bima nchini hususani kwa Mawakala wa Bima. Aidha, Kamishna wa Bima alitumia fursa hiyo kuwajulisha Mawakala wa Bima juu ya Mamlaka kuendelea kusogeza huduma kwa Mawakala na watoa huduma wengine wa Bima kwa kuongeza ofisi za kanda ambazo ni; Kanda ya Kusini yenye ofisi zake Mkoa wa Lindi ikihudumia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, Kanda ya mashariki inayosimamia mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Ruvuma, pamoja na Kanda ya Magharibi itakayokuwa ikihudumia Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Kamishna wa Bima alihitimisha kwa kusema kuwa Mamlaka itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa soko la Bima ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo mbalimbali itakayoleta ufanisi katika sekta ya Bima.

Pichani ni Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware aliyesimama akijibu maswali mbalimbali wakati wa mkutano huo, waliokaa kushoto ni Meneja wa Mamlaka Kanda ya Mashariki Bw. Frank Shangali, na Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakala wa Bima Tanzania (IAAT) Bw. Sayi John Daudi.