Kamishna wa Bima amefanya mkutano na waandishi wa Habari katika Ofisi za Mamlaka ya Bima Zanzibar
Leo tarehe 02/08/2023 Kamishna wa Bima amefanya mkutano na waandishi wa Habari katika Ofisi za Mamlaka ya Bima Zanzibar. Lengo la mkutano huo ni kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na matokeo ya ukaguzi wa vyombo vya moto Wilaya ya Mjini Unguja. Ukaguzi huo ulifanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA) kuanzia tarehe 25 hadi 31 Julai 2023 Unguja kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya mjini Unguja Mhe. Rashid Msaraka, Jeshi la Polisi na vikosi Maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa umma Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware amesema wakala wa Bima "TABASAM CENTRAL AGENCY COMPANY LTD" alikutwa na hatia ya kutoa huduma za Bima kinyume na Sheria ya Bima Sura 394, na Waraka namba 093/2021 kwa kukaa na Ada za Bima bila ya kuziwasilisha kwa kampuni ya bima. Kutokana na makosa hayo Kamishna wa Bima amefunga rasmi wakala wa Bima TABASAM kutojihusisha na biashara ya bima Nchini na kuwasilishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria kwa hatua zaidi.
Aidha Kamishna wa Bima ametoa wito kwa watoa huduma za bima Nchini kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya bima ili kuwa na soko la bima lisilokuwa na udanganyifu lenye kufuata weledi na ushindani.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA.