Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Benki ya NBC wameandaa semina ya mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya dhamana (Trust Account)
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Benki ya NBC leo tarehe 01.08.2023 wameandaa semina ya mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya dhamana (Trust Account) kwa kampuni za bima. Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam kuanzia saa 05:00 asubuhi.
Semina hiyo ilifunguliwa na Mgeni rasmi Dkt. Baghayo A. Saqware Kamishna wa Bima akiambatana na baadhi ya wakurugenzi na watumishi wa Mamlaka ya Uismamizi wa Bima Tanzania (TIRA). Aidha, wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw. Theobald Sabi pamoja na Wakurugenzi Watendaji Wakuu, Maafisa Wakuu wa Fedha wa kampuni za Bima wamehudhuria semina hiyo ya mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya dhamana (Trust Account).
Akitoa hotuba yake, Mgeni rasmi Dkt. Saqware ameipongeza benki ya NBC kwa kuwa benki ya tatu kutekeleza mchakato wa uanzishwaji wa Akaunti ya dhamana ya bima yaani (Trust Account). Pia aliwapongeza Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Wakuu wa Fedha wa makampuni ya bima nchini kwa kuhudhuria semina hiyo
Dkt. Saqware amesema uanzishwaji wa akaunti hiyo ya dhamana ya bima ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kuendana na matakwa ya kisheria na udhibiti yaliyowekwa na Mamlaka ya Uismamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Vile vile amesema utaratibu uliokuwa ukitumika mwanzoni katika usimamizi wa dhamana ya bima haukuwa mzuri jambo ambalo lilipelekea Mamlaka kushindwa kusimamia vizuri amana hizo pindi ziliporejeshwa kwa makampuni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) baada ya kuiva.
Amesema kuwa kampuni nyingi za bima zilikuwa zikitumia fedha za amana ya Akiba katika matumizi mengine, pasipo kupata idhini ya TIRA hivyo kupelekea kuingia katika changamoto ya ukwasi, na wakati mwingine kushindwa kulipa fidia kwa wateja kutokana na fedha kuwekezwa katika miradi mingine.
Aidha, alibainisha kuwa uamuzi wa kufungua akaunti ya dhamana ya bima katika benki za biashara ni mwarobaini wa changamoto hiyo, kwani sasa Mamlaka (TIRA) itaweza kusimamia moja kwa moja fedha hizo za amana za akiba, jambo ambalo si tu litaimarisha usimamizi, bali pia litaboresha maendeleo ya sekta ya fedha.
Dkt. Saqware alihitimisha kwa kusema chimbuko la akaunti hiyo ya dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 kifungu namba 20 inayozitaka kampuni za Bima kuweka amana za usalama angalau 50% ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima na hatimaye kuwataka washiriki wote hususani Maafisa Wakuu wa Fedha wa kampuni za Bima kuzingatia mafunzo yatakayotolewa na benki ya NBC na kuwakaribisha washiriki wote katika ofisi za Mamlaka (TIRA) Makao makuu Dodoma, Kanda ya Mashariki Dar es Salaam, Kanda ya kusini Lindi, Kanda ya kasikazini Arusha, Kanda ya ziwa Mwanza, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, Kanda ya magharibi Tabora, Kanda ya kati Dodoma, na Ofisi ya TIRA Zanzibar.