ZIARA YA UTOAJI ELIMU YA BIMA YA AFYA ZANZIBAR YAANZA RASMI
Ziara ya utoaji elimu kuhusu bima ya afya Visiwani Zanzibar imeanza rasmi leo Agosti 13, 2024 ambapo Ujumbe kutoka TIRA unaoongozwa na Naibu Kamishna Bi. Khadija Said ulitembelea Mkoa wa Kaskazini Unguja na kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Mhe. Othman Ally Maulid na Baadae kukutana na Mkuu wa Mkoa Mhe. Rashid Hadid Rashid ambapo pia Masheha zaidi ya Sabini walipatiwa uelewa kuhusu bima ya afya na bima nyingine ikiwemo bima ya kilimo.
Awali Naibu Kamishna Bi Khadija Said, akifanya Wasilisho kwa Mkuu wa Mkoa, wa Kaskazini Unguja Mhe. Rashid Rashid amesema lengo la Ziara ya TIRA ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi ambao wamesaini sheria ya bima ya Afya kwa wote.
Aidha amewakumbusha kwamba tarehe 19 Novemba 2023, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisaini sheria ya bima ya afya kwa wote namba 13 ya mwaka 2023 ambapo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anakata bima ya afya kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwenye hospital na vituo vya afya nchini.
Nae Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi alisaini Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar ya mwaka 2022. Sheria hizi zote zinalenga kuhakikisha kwamba kila raia na wageni wote ndani ya nchi wanapata huduma za uhakika za afya kwa kutumia bima ya afya.
Naibu Kamishna akasisitiza pia umuhimu wa Viongozi wa serikali wakiwemo Masheha kuwa na uelewa wa maswala ya bima ili kwa nafasi zao kueneza pia uelewa huo kwa wananchi walio wengi zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Rashid ameipongeza TIRA kwa juhudi inazochukua ya kutoa elimu kuhusu maswala ya bima na kuwasihi waendelee kutoa elimu hiyo mara kwa mara kwa kuwa bima ni jambo lenye manufaa hivyo watu wakilielewa vizuri idadi ya watumiaji itaongezeka. Ameunga mkono pia wazo liliotolewa na TIRA la kuwepo na Ofisa maalum atakaekuwa anashughulikia maswala ya bima kwa kupeleka taarifa za mara kwa mara TIRA.