TIRA yazindua Ofisi Kanda ya Magharibi
Leo Desemba 2, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Burian amezindua rasmi ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) iliyopo Mkoani Tabora.
Ofisi hiyo ya TIRA inahudumia pia mikoa ya Kigoma na Katavi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Dkt. Batilda amesema uwepo wa ofisi ya TIRA mkoani Tabora itaamsha ari kwa Wananchi wa mkoa huo kukata bima za aina mbali mbali ikiwemo bima za kilimo, Mifugo na moto.
Nae Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware amesema ni adhma ya TIRA kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanakua na uelewa kuhusu Bima na kwamba hadi kufikia 2030 asilimia 80 ya watanzania wawe wamepata elimu kuhusu Bima.
Upande wake Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Said amewahakikishia wananchi wa ukanda wa Magharibi kuwa TIRA itawapatia huduma stahiki ili kurahisisha mahitaji kuhusu bima yanapatikana kwa wakati.
Hafla ya uzinduzi wa ofisi za TIRA zimehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tabora wakiwemo wa chama na serikali, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja waendesha Bodaboda.
Kanda hiyo ya Magharibi inasimamiwa na Meneja wa TIRA Dkt. Emmanuel Lupilya ambae anaendelea kutoa elimu ya bima kupitia makundi mbalimbali.