Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA YAKUTANA NA MAKATIBU WAKUU NA NAIBU MAKATIBU WAKUU SMZ
03 Apr, 2024
TIRA YAKUTANA NA MAKATIBU WAKUU NA NAIBU MAKATIBU WAKUU SMZ

Machi 22, 2024 Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imefanya Mkutano na Makatibu Wakuu pamoja na Manaibu Katibu Wakuu  wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambapo Mgeni Rasmi alikua ni Mhandisi Zena Ahmed Said Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi SMZ

Kikao hicho kilichowakutanisha pia Watendaji Wakuu wa NIC, ZIC, EARE, PDB na Msajili wa Hazina  kilipokea matokeo ya tathmini iliyofanywa na TIRA kuhusu ukatiwaji wa  Bima wa Mali za Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akifanya Wasilisho lake Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware amesema, Kwa upande wa Bima za Vyombo vya Moto na Bima za Afya, SMZ imefanya  vizuri kwa zaidi ya asilimia 80 na kuwaomba watendaji hao wakuu wa Serikali kuendelea kutilia mkazo kwenye upande wa bima nyingine kwani zinasaidia kukinga mali za serikali dhidi ya Majanga mbalimbali.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Balozi wa Bima amewataka Makatibu hao kufanya tathmini ya mali zote zilizopo kwenye Wizara zao na pia kufanya tathmini ya gharama za malipo ya bima ili kusaidia kufanya maamuzi yenye tija. Ameongeza kuwa ni vyema pia watendaji hao kupatiwa uelewa mpana juu ya aina mbalimbali za bima.

Awali akitoa neno la Ukaribisho Naibu Kamishna wa Bima Tanzania Bi Khadija Said amesema, Mamlaka imejidhatiti kutoa ushirikiano ili kurahisisha huduma za bima Visiwani Zanzibar na kwamba hivi karibuni TIRA itafungua ofisi nyingine Pemba na ofisi nyingine Unguja.

Kikao hicho  ni mfululizo wa utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka yanayolenga kukuza soko la bima nchini.

TIRA kwa soko salama la bima