TIRA TUMETEKELEZA: Mafanikio na Mabadiliko katika Sekta ya Bima kwa mwaka 2024
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA
2024 MWAKA WA MAFANIKIO NA MABADILIKO KATIKA SEKTA YA BIMA
Mwaka 2024 umeleta mafanikio makubwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), huku ikijidhihirisha kama kiongozi wa mageuzi ya sekta ya bima nchini. Kwa usimamizi na ushirikiano wa karibu na wadau wa sekta, TIRA imechukua hatua madhubuti za kuimarisha soko la bima, kuboresha mifumo, na kuongeza uelewa wa bima miongoni mwa Watanzania.
Elimu na Ushirikiano wa Kijamii
TIRA imeendelea kusimamia utoaji wa elimu ya bima kwa makundi mbalimbali ya jamii. Kupitia programu maalum za kuelimisha, mamlaka imefanya mikutano na wamiliki wa mabasi, waendesha bodaboda, na makundi mengine muhimu katika sekta ya usafirishaji. Hii imelenga kuwajengea uwezo wa kuelewa bima na faida zake, huku ikipunguza changamoto zinazoikumba sekta hiyo.
Katika kuimarisha ufahamu wa bima kwa makundi maalum, TIRA imekuwa mstari wa mbele kufanikisha usawa wa kijinsia na kujumuisha watu wenye mahitaji maalum. Maonesho mbalimbali ya kitaifa kama vile Sabasaba na Nane Nane yamekuwa jukwaa la kuelimisha kuhusu bima kwa lugha nyepesi na njia zinazovutia.
Mageuzi ya Kisera na Kisheria
Kwa mwaka huu, TIRA imezindua miongozo na sera zinazolenga kuboresha mazingira ya kisheria kwa watoa huduma za bima na wateja. Hii ni pamoja na kuongeza uwajibikaji wa kampuni za bima kuhakikisha fidia zinalipwa kwa wakati. Kwa kushirikiana na taasisi za serikali, TIRA imehakikisha kwamba mali za umma zinalindwa ipasavyo kupitia bima, hatua inayochochea uwajibikaji wa kifedha na kupunguza mzigo wa gharama kwa serikali. Mfano wa miongozo iliyotolewa kwa mwaka 2024 ni pamoja Miongozo ya bidhaa za bima, Miongozo ya Wakaguzi wan je wanaohudumia sekta ya bima na muongozo wa ukokotoaji na ukusanyaji wa tozo za ada za bima.
Ubunifu katika Sekta ya Bima
Mwaka 2024 pia umeona kuzinduliwa kwa huduma mpya za bima zinazolenga mahitaji ya kipekee ya wateja. Mojawapo ya mafanikio makubwa ni kuzinduliwa kwa huduma za Takaful, ambazo zinafuata misingi ya Shariah. Uzinduzi huu umeimarisha zaidi utoaji wa huduma zinazojumuisha makundi tofauti ya dini na tamaduni.
Maonesho ya Kimataifa na Ushiriki wa TIRA
Katika maonesho makubwa ya Sabasaba 2024, TIRA na wadau wa sekta ya bima ilizindua "Kijiji cha Bima," ambapo wananchi walipata fursa ya kujifunza kuhusu huduma za bima kupitia njia rahisi na shirikishi. Kijiji hiki kimekuwa mfano wa ubunifu wa kuifikisha bima kwa kila mmoja, huku kikionyesha dhamira ya TIRA ya kuimarisha elimu ya bima kwa Watanzania wote.
Uzinduzi wa Taarifa ya utendaji wa soko la bima kwa maak 2023
Tukio hili lilifanyika mwezi Novemba 2024 na kuhudhuria na watu zaidi ya 400 huku watu zaidi ya 1000 wakifuatilia mbashara kupitia mtandao wa YouTube wa Mamlaka. Tarifa hii imeonesha kukua kwa soko kwa kiwango kikubwa kama ifuatavyo;
Ada za Bima (Gross Premiums Written - GPW) zimepanda kwa asilimia 7.4 hadi kufikia TZS trilioni 1.24, kutoka TZS trilioni 1.17, watoa huduma za bima wameongezeka kwa asilimia 33, na kufikia 1,549 ikilinganishwa na 1,164 mwaka uliopita. Aidha, madai ya bima yaliyolipwa yameongezeka kwa asilimia 25.5, hadi kufikia TZS bilioni 488.2 kutoka TZS bilioni 389.
Kiwango cha mali za bima kimeongezeka kutoka TZS trilioni 1.7 hadi kufikia TZS trilioni 2.15 huku uwekezaji pia ukiongezeka hadi TZS trilioni .1.27 kutoka TZS trilioni 1.17. Fursa za ajira zimeongezeka kwa asilimia 34.1, ambapo jumla ya ajira 5,595 zimekodiwa mwaka 2023. Aidha, kiwango cha ubakizaji wa bima za kawaida (general insurance retention) kimeongezeka kutoka asilimia 49.4 hadi asilimia 55.5 huku kiwango cha ubakizaji wa bima za maisha kikiwa ni asilimia 83.2.
Utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Kwamujibu wa Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, inatoa haki ya msingi ya kila Mtanzania kuwa na bima ya afya bila kujali kama wanatoka katika sekta rasmi au isiyo rasmi.Katika kutekeleza hilo TIRA imepewa jukumu la kisheria kusimamia skimu zote za bima ya afya ili kuhakikisha watoa huduma wanafuata taratibu sahihi za usajili wa wanachama na pia kufuatilia utekelezaji wa huduma zinazotolewa ili huduma zinazotolewa ziendelee kuwa bora na za haki kwa wanachama walio kwenye skimu husika.Mwaka 2024 kanuni kwa ajili ya kuanza kwa utekelezaji wa sheria hiyo zimetoka ambapo zinasisitiza juu ya usajili wa wanachama kwa uwazi na kuhakikisha michango inawasilishwa kwa wakati. Katika kuchangia juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za afya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kushirikiana na wadau imetoa kadi za bima ya fya 3000 kwa watanzania wenye uhitaji ikiwa ni utekelezaji wa kauli ya Kamishna wa Bima Tanzania aliyoitoa ya kuchangia kadi za bima kwa watanzania 10,000 ili waweze kupatiwa matibabu.
Maono ya TIRA kwa Soko Salama la Bima
Kwa mwaka 2024, TIRA imeendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali inayowezesha usajili wa bima, ulipaji wa fidia kwa wakati, na usimamizi wa masuala ya kisheria kwa uwazi zaidi. Mfumo huu unalenga kujenga imani miongoni mwa wateja na watoa huduma, huku ukihamasisha ukuaji wa sekta ya bima nchini.
Kauli ya Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware
“Sekta ya bima ni nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa. Tunaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha huduma za bima zinawafikia Watanzania wote kwa uwazi, ubora, na ufanisi,” anasema Dkt. Saqware.
Kwa mafanikio haya ya mwaka 2024, TIRA imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama mshirika wa maendeleo ya taifa. Mamlaka imeonyesha kuwa bima si tu kinga dhidi ya majanga, bali pia ni chombo muhimu cha kuboresha maisha na uchumi wa kila Mtanzania.