Tira ya zindua akaunti ya dhamana ya Bima
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (TIRA), kutekeleza mchakato wa uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima (Trust Account).
Mafuru ametoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya utekelezaji wa akaunti hiyo kwa Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Wakuu wa Fedha wa makampuni ya bima nchini yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.
Mafuru amesema uanzishwaji wa Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kuendana na matakwa ya kisheria na udhibiti yaliyowekwa na TIRA.
Mafuru amesema utaratibu uliokuwa ukitumika mwanzoni katika usimamizi wa dhamana ya bima haukuwa mzuri jambo ambalo lilipelekea TIRA kushindwa kusimamia vizuri amana hizo pindi ziliporejeshwa kwa makampuni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) baada ya kuiva.
Amesema kuwa kampuni nyingi za bima zilikuwa zikitumia fedha za amana ya Akiba katika matumizi mengine, pasipo kupata idhini ya TIRA hivyo kupelekea kuingia katika changamoto ya ukwasi, na wakati mwengine kushindwa kulipa fidia kwa wateja kutokana na fedha kuwekezwa katika miradi mingine.
Mafuru alibainisha kuwa uamuzi wa kufungua Akaunti ya Dhamana ya Bima katika benki za biashara ni mwarobaini wa changamoto hiyo, kwani sasa TIRA itaweza kusimamia moja kwa moja fedha hizo za amana za akiba, jambo ambalo si tu litaimarisha usimamizi, bali pia kuboresha maendeleo ya sekta ya fedha.
Akizungumza katika warsha hiyo, Kamishina wa Mamlaka ya Bima, Dkt. Baghayo Saqware amesema chimbuko la Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 inayozitaka Kampuni za Bima kuweka Amana za Usalama angalau asilimia 50 ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima.
Dkt. Saqware amesema mwaka jana Mamlaka kwa kushirikiana Chama cha Watoa Huduma za Bima (ATI), walikubaliana kuandaa Mwongozo wa Uwekazaji wa Usimamizi wa Ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.
Akitoa taarifa za utendaji wa sekta ya bima, Dkt. Saqware alimjulisha Naibu Katibu Mkuu kuwa sekta hiyo imeendelea kukua kulinganisha na miaka iliyopita. Amesema mwaka jana mauzo ya bima yaliongezeka kwa asilimia 25 kufikia Shilingi Trilioni 1.146 kulinganisha na mauzo ya 2021. Aidha, alibainisha kuwa malengo ya mwaka huu ni kufikia Shilingi Trilioni 1.5.
CAPTION
Kamishna wa Bima Dk. Baghayo Abdallah Saqware akitete jambo na Naibu Katibu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru katika uzinduzi wa Mafunzo ya Utekelezaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Issa Said akifuatilia mafunzo maalum ya Utekelezaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima wakifuatilia mafunzo maalum ya Utekelezaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.