TIRA YACHANGIA ZAIDI YA MILIONI 20 KUBORESHA HOSPITALI YA RUFAA YA AMANA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imeshiriki kwenye halfa ya Harambee iliyopewa jina la 'Rafiki wa Amana Dinner Gala 2024' iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Amana ambapo mgeni rasmi alikua Mhe. George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akihudhuria hafla hiyo, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amesema kuwa TIRA imechangia zaidi ya milioni 20 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti, wajawazito pamoja na kununua vifaa tiba ili kuboresha Hospitali ya Rufaa ya Amana ikiwa ni moja ya hatua za kushiriki kijamii katika kuhakikisha watanzania wanapata huduma za afya za uhakika.
Dkt. Saqware ameongeza kuwa nia ya Mamlaka ni kuona huduma za afya zinazotolewa ni zenye ubora na zenye uhakika. Hatua hii ya kuchangia kwenye kwenye sekta ya afya pia kutaiendeleza Sekta ya Bima kwakua watumiaji wa huduma za afya pia ni watumiaji wa bima. Matarajio ni kwamba kupitia Bima ya Afya kwa Wote (UHI) na uboreshaji wa hospitali kama Amana, wananchi wengi zaidi wataweza kupata huduma za afya kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Aidha, jitihada hizi zinachochea lengo la serikali la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kupitia mfumo wa bima, ambao unatoa fursa kwa wananchi kulipa gharama za matibabu kwa usalama na kuondoa mzigo wa gharama zisizotarajiwa.
TIRA inaamini kuwa afya bora inachangia katika maendeleo ya jamii, na hivyo, Mamlaka inajitolea kuendelea kushirikiana na sekta ya afya katika kampeni na miradi inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi. "Lengo letu ni kuona kila Mtanzania anapata huduma bora za afya na kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma kutokana na kukosa uwezo wa kugharamia matibabu," amesema Dkt. Saqware.