TIRA YAFIKISHA ELIMU YA BIMA SONGWE, ULIPO TUPO
Katika jitihada za kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa (FYDP II-2020-2025) pamoja na Mpango Mkuu wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDMP-2020-2030), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa utoaji elimu ya bima kwa umma. Hii ni hatua muhimu kuelekea maendeleo ya sekta ya bima nchini.
TIRA imejizatiti kuongeza kasi ya utoaji elimu ya bima kwa umma, taasisi, na viongozi wa serikali kwa lengo la kuleta maendeleo kwenye sekta ndogo ya bima. Kwa kushiriki na kuandaa mikutano na hafla mbalimbali, TIRA inalenga kutoa elimu ya bima kwa taasisi, makundi mbalimbali, viongozi wa serikali, na wananchi kwa ujumla.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, TIRA imepanga kuwatembelea wakuu wa mikoa na wilaya za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa malengo mahsusi ikiwemo: Kuwajulisha wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu umuhimu na hatua za utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Kutambulisha Ofisi za Kanda za TIRA ili kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa majukumu na kutoa elimu ya bima kwa wakuu wa mikoa na wilaya ili waweze kuhimiza matumizi ya bidhaa na huduma za bima katika jamii zao na hatimaye kuweka misingi ya ushirikiano mzuri na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kulinda haki za watumiaji wa bima na kuhakikisha kuwa huduma za bima zinawafikia wananchi kwa urahisi na uwazi.
Katika hatua ya kutekeleza azma hii, Mamlaka kupitia Ofisi ya Kamishna wa Bima na ujumbe wake wamemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Daniel Chongolo ili kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wanasongwe.
Aidha Mhe. Chongolo amesisitiza juu ya umuhimu wa Mamlaka kuendelea kuwafikia watanzania kwa mbinu mbalimbali ambazo zinaeleweka kwa urahisi. Jitihada zinazoendelea kufanyika ili kufikisha elimu ya bima ziungwe mkono na viongozi wa ngazi husika ili wawe mabalozi makini kwa wananchi na hatimaye kuhakikisha elimu ya bima inawanufaisha hasa bima za kilimo na za afya.
Songwe ni moja ya Mikoa wenye muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kutokana na uwepo wa bandari kanda ya juu kusini na ni eneo ambapo mizigo kutoka nchi jirani inapitishwa, pia uwepo wa shughuli za kilimo na wachimbaji wa madini ambao hawana elimu ya bima. Hivyo, ni vema elimu ya bima iwafikie wanasongwe ili waweze kujikinga wao na mali zao.
Ziara hii inaanza leo tarehe 5 Agosti 2024 na itahusisha kanda ya nyanda za juu kusini, kanda ya kusini, pamoja na mkoa wa Morogoro uliopo kanda ya mashariki. Hatua hii ni muhimu katika kudumisha uhusiano na taasisi mbalimbali na kulinda haki za watumiaji wa bima nchini.