Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA yashiriki mkutano wadau wa elimu Dodoma - "Kateni bima kulinda afya na mali" - Dkt. Saqware
21 Mar, 2025
TIRA yashiriki mkutano wadau wa elimu  Dodoma - "Kateni bima kulinda afya na mali" - Dkt. Saqware

Kauli mbiu hii imetekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushiriki na kudhamini tuzo katika Mkutano wa Wadau wa elimu ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Sitaki Sinyamule tarehe 20 Machi 2025 ukiwa na lengo la kutunuku tuzo  kwa walimu, wanafunzi, shule na Wilaya, zilizofanya vizuri katika mitihani ya darasa la Nne, darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita kwa mwaka 2024 katika Mkoa wa Dodoma.

Tuzo hizo zimekua hamasa kubwa kwa wale wote waliofanya vizuri kwani wamezifurahia na pia zimekuwa chachu kwa wengine katika kuhakikisha wanaongeza bidii katika mitihani yao na hivyo kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla ambapo Sekta ya elimu nayo itazidi kuwa bora.

Katika Mkutano huo uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu zaidi ya elfu mbili, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware alipata nafasi ya kueleza Majukumu ya Mamlaka pamoja na manufaa ya bima. 

Kamishna  Saqware aliwaeleza wadau hao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma  kwamba walimu, wanafunzi na wananchi wote wakate bima kwa ajili ya kujilinda afya zao, kulinda mali zao na za Serikali kwa ujumla. Lakini pia aliwahamasisha wadau hao kuwa bima ni sehemu ya kujiongezea kipato kwa  kuwa wakala wa bima.

Mgeni Rasmi wa Mkutano huo alikuwa Dkt. Doto Mashaka Biteko ambaye kutokana na majukumuj mengine ya kitaifa hakufanikiwa kufika na badala yake aliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Sitaki Sinyamule.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA