TIRA yatoa elimu ya bima kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia kanda ya Mashariki imetoa elimu ya bima kwa watumishi mbalimbali wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa bima na matumizi yake kwa watumishi hao.
Mamlaka imeshirikiana na wadau wake mbalimbali kutoa mafunzo katika semina hiyo wakiwemo wawakilishi wa NHIF, CRDB Bima na NIC.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi Bw. Lawrance P. Malangwa aliishukuru Mamlaka kwa kufikisha elimu hiyo ambayo amesema itawasaidia kama taasisi lakini pia kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja na kuwataka watumishi kuitumia fursa hiyo kujifunza na kutumia bidhaa za bima.
Aidha Meneja wa TIRA kanda ya Mashariki Bw. Zakaria Muyengi alifungua uwasilishwaji wa mada kwa kuelezea uazishwaji wa Mamlaka, majukumu yake na hali ya soko la bima hapa nchini. Lakini pia amesisitiza mambo mawili kwa watumishi hao ikiwa ni kuelewa kuhusu bima ya maisha kuitumia na umuhimu wake kwa familia husika. Jambo la pili amesisitiza lengo la Mamlaka (Ofisi ya Kanda ya Mashariki) kuwa na mtumishi maalumu anayetoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, atakayeshughulikia malalamiko yahusuyo bima yanayoletwa katika ofisi hizo na wananchi ili kurahisisha mawasiliano na uwasilishwaji wa haraka kwa Mamlaka,kanda husika.
Afisa Bima Ndg. Joseph Mfoi pia ametoa elimu ya umuhimu na aina za bima na kusisitiza watumishi hao kuhakikisha wanalinda afya, mali na uwekezaji ili kurudi katika hali ya kawaida pale wanapopatwa na majanga.
Mada nyingine iliyowasilishwa ni pamoja na Taratibu za Kushughulikia Malalamiko ya Wateja wa Bima na Afisa Sheria Renatus Kaijage ambapo alieleza kuhusu hatua za kufuata na njia za kutumia kufikisha malalamiko ikiwemo kufikisha barua kwa njia ya barua pepe au kufika katika ofisi za Mamlaka za karibu lakini pia alisisitiza utaratibu wa kutuma malalamiko kupitia njia ya tovuti ambao unafanyiwa kazi kuanza rasmi.
Pia Mwakilishi wa NHIF, Bi. Elizabeth Albin alisema chini ya Usimamizi wa TIRA, NHIF imejipanga kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote kwa na kwa sasa imeboresha mifumo yake ya uhakiki wa kadi kabla ya matibabu, lakini pia usajili wa wanachama kuanza kufanyika kwa njia ya mtandao na pia mifumo ya NIDA na NHIF imejumuishwa kurahisisha huduma. Nae Bi. Eliza Chaki kutoka NIC amesisitiza watumishi wao kujipanga kwa kupunguza baadhi ya mambo yasiyo ya lazima ili kujiwekea akiba na kuweza kuwa na bima ya maisha itakayokinga familia zao baada ya kifo.
TIRA kanda ya Mashariki inayodumu mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani na Morogoro imekuwa ikitoa mafunzo kwa watumishi wa serikali, taasisi binafsi, vyama vya ushirika, makundi ya wajasiriamali na wafanyabiashara mbalimbali lengo likiwa kupenyeza elimu ya bima ili wananchi waweze kutumia na kujikinga na umaskini baada ya majanga.
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA