Ukuaji Soko La Bima Umechangiwa Na Uwekezaji Bora Na Soko La Bima Imara – Naibu Waziri Fedha
Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2023 Mhe. Hamad H. Chande; Naibu Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameeleza kufurahishwa na ukuaji wa soko la bima hapa nchini.
“Nimeshuhudia ongezeko la wasajiliwa utoaji huduma za bima ukiongezeka kutoka watu elfu moja mia moja na sitini na tano (1165) kwa mwaka 2022 hadi watu elfu moja mia nne na sabini na mbili (1472) kwa mwaka 2023, hili limechangiwa na uwekezaji mzuri na soko la bima imara” amesema.
Mhe. Chande pia ameeleza ripoti hiyo inatoa hali halisi, picha ya wazi na taswira ya soko la bima nchini na kuipongeza Bodi ya Taifa ya Bima, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) pamoja na kamati ya maandalizi kwa uandaaji wa Taarifa hiyo muhimu ikizingatiwa pia TIRA ni miongoni mwa sekta za fedha zinazochangia kuongeza pato ya Serikali.
Naibu Waziri pia aliipongeza Mamlaka kwa kujenga mahusiano ya karibu na mazingira wezeshi kwa watoa huduma za bima na kusisitiza uendelevu wa mafanikio hayo kwasababu Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira bora ya uwekezaji. Lakini pia alitoa angalizo kwa Mamlaka kufatilia uwepo wa bima katika sekta ya michezo ambapo vijana wengi watafikiwa katika huduma za bima, lakini pia Mamlaka kuendelea kuongeza kasi ya matumizi ya kidigitali ili kurahisisha utolewaji wa huduma za bima.
Zaidi pia alizitaka kampuni za bima kufanya kazi kwa uaminifu kwasababu Serikali imeziamini kwa kutoa leseni ili waweze kufikisha huduma bora kwa watanzania na kusisitiza uwekezaji zaidi katika sekta za mafuta na gesi, usafiri, utalii, kilimo, mifugo, uvuvi na nyinginezo na mwisho alitoa neno kuhusu bima ya afya kwa wote;
“Bima ya Afya kwa Wote ni mkakati utakaoleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwa watanzania”
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA