Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
USHIROMBO KUNUFAIKA NA BIMA ZA AFYA ELFU KUMI
14 Sep, 2024
USHIROMBO KUNUFAIKA NA BIMA ZA AFYA ELFU KUMI

USHIROMBO KUNUFAIKA NA BIMA ZA AFYA ELFU KUMI

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewafikia jumuiya ya waislamu zaidi ya elfu tano (5,000) wa Kata ya Ushirombo, Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita leo Septemba 13, 2024 katika tukio maalum lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ambapo mgeni rasmi alikua Naibu Chief Kadhi (Kaimu Mufti ), Sheikh Ally Hamis Ngeruko. 

Zoezi hilo lililenga kutoa elimu ya bima itakayowajengea wakazi hao wa Bukombe uelewa wa umuhimu wa Bima ya Afya na kuwamasisha kutumia huduma hiyo kufuatia ahadi ya Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware ya kutoa Bima za Afya elfu kumi (10,000). 

Katika awamu hii ya kwanza zinatarajiwa kutolewa Bima za Afya elfu moja (1,000) ambazo tayari zimeshachakatwa na zimeshaandaliwa kugawiwa huku zinazosalia elfu tisa (9,000) kugawiwa katika awamu endelevu. Bima hizo hazitabagua na zitatolewa mahususi kwa walengwa ambao hasa wana uhitaji wakiwemo wazee, walemavu, wasio na uwezo, wanawake na watoto bila kujali dini, rangi wala kabila.  

Akisisitiza umuhimu wa kuwa na bima ya afya Sheikh Ngeruko amesema,” Gharama za kadi hizo za bima zinasimamiwa na Mufti pamoja na TIRA kwa kipindi cha mwaka mzima, hivyo wale watakaopewa kadi hizo wataweza kunufaika na huduma za afya ama matibabu stahiki kwa kipindi cha mwaka mzima bila kugharamia chochote. Nawakumbusha pia bima hii haibagui, kwakua wote ni binaadamu tunapoumwa wote tunastahili kupata matibabu, kwa hiyo bima hii itatolewa hata kwa wale wasiokua waislamu”. 

Akitoa elimu ya Bima mbele ya hadhira hiyo, Afisa Bima kutoka TIRA, Bw. Ayoub Mremi amesema hatua hii inadhihirisha mipango endelevu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kama msimamizi wa sekta ya bima nchini katika kuhakikisha jamii haziachwi nyuma na wote wanakua sehemu muhimu ya maendeleo haya kwa mustakabali wa sekta nzima. Ameeleza kuwa suala la bima ya afya limekua ni jambo linalogusa jamii mbalimbali bila kujali tofauti zao na hata watu binafsi. Bima hizo zitakazotolewa zitasadia kumkinga mtu binafsi na hata familia kwa pamoja pale maradhi yanapoibuka bila kutarajia kunakua na uhakika wa kupata matibabu.