Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
UZINDUZI WA UMOJA WA MAWAKALA WA BIMA WANAWAKE, WAJIPANGA KULETA MAGEUZI SEKTA YA BIMA
05 Sep, 2024
UZINDUZI WA UMOJA WA MAWAKALA WA BIMA WANAWAKE, WAJIPANGA KULETA MAGEUZI SEKTA YA BIMA

WANAWAKE SEKTA YA BIMA WAJIPANGA KUWEKEZA KULETA MAGEUZI 

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) yahudhuria halfa ya Uzinduzi wa Umoja wa Mawakala wa Bima Wanawake Tanzania (UMABIWATA) leo Septemba 05, 2024 jijini Arusha.

Tukio hilo limehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa ambaye alikuwa mgeni rasmi na wengine wakiwemo Kampuni mbalimbali za bima na wadau wengine katika Sekta.

Kupitia zoezi hili Mhe. Felician ameeleza kuwa umoja huu unaakisi maendeleo na mafanikio ya jitihada zinazofanywa na Rais ya Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mamlaka husika inayosisamia Sekta ya Bima nchini TIRA. Kwakua dharura na majanga hayatokei kwa taarifa, ni vema jamii zieendelee kuelimishwa na kuhamasishwa umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kutumia huduma mbalimbali za bima.

Akiiwakilisha Mamlaka ya Usimami wa Bima, Meneja wa Kanda ya Kaskazini, Bw. Bahati Ogolla amesema kuanzishwa kwa UMABIWATA ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi sawa na fursa ya kuingia na kufanikiwa katika sekta ya Bima. Chama hiki kimedhamiria kuongeza tija na wigo katika utoaji huduma kwenye soko la Bima Tanzania, ili kuwezesha wanawake wengi zaidi kuwekeza kwa kua mawakala wa Bima ili kuongeza nguvu kwenye Soko la Bima.

Aidha, kupitia programu mbalimbali wanawake hawa wataweza kusaidiana kitaalamu katika maswala yanayohusu Bima ili hatimaye kusaidiana wakati wa shida kama vile kufiwa, ugonjwa ama kuunguliwa na moto. Pia, wataweza kukua kiuchumi, kuboresha hali za kijamii kwa kutoa ajira mbalimbali, kutoa elimu ya bima, kuongeza wigo wa kuwafikia Watanzania, pamoja na kuchangia ukuaji wa soko la Bima..

Katiba wa UMABIWATA, Bi. Edina Mgage amesema kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na makampuni mbalimbali ya bima, wadau mbalimbali na Mamlaka inayosimamia  Sekta. Bi. Mgage amesema,”Lengo letu hapo baadae ni kufungua kampuni ya Bima ya Wanawake ambayo itakua ya kwanza Tanzania na Africa tukifuata mfano wa benki ya wanawake tanzania (Tanzania Women’s Bank). Ndoto yetu kama wanawake wenye uthubutu ni kuendelea kuwa mstari wa mbele kuziinua jamii zetu ili ndoto zetu zisipeperuke au kubaki kuwa nadharia tu bali tuwe chama chenye kuacha alama katika soko letu la bima nchini”.

Bw. Ogolla ameeleza kuwa"Ni matumaini yetu kwamba chama hiki kitaenda kuongeza chachu zaidi ya ushiriki mkubwa wa wanawake katika utoaji huduma za uwakala wa Bima kwa njia za kawaida, na njia mbadala kulingana na ukuaji wa teknolojia kwa kupitia mifumo mbalimbali, na hivyo kwenda kufikia mpango wa asilimia 50% ya watanzania wanaotumia huduma na bidhaa za Bima ifikapo 2030". 

Mafanikio makubwa ya Sekta ya Bima hayataweza kupatikana pasipo ushirikiano imara na ushirikishwaji wa wadau wengine muhimu wa sekta ndogo ya bima. Lengo kubwa kama Mamlaka ni kuwa na soko la bima lisilo na udanganyifu, lenye kufuata weledi na soko la bima lenye kuleta tija kwa Taifa.