WAKULIMA SUMBAWANGA WAPEWA SOMO UMUHIMU BIMA YA KILIMO
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Kanda ya Ziwa Tanganyika imetoa elimu ya bima kwa wakazi wa mji wa Sumbawanga Octoba 04 2024. Katika mkutano huo uliofanyika mjini hapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndg. Msalika R. Makungu akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo.
Timu ya Mamlaka ilikwenda na ujumbe muhimu wa kuwahamasisha wakulima kukata bima ya mazao ambapo wengi wanafanya kilimo cha zao la biashara la mahindi na ikiwa msimu wa kilimo upo mbioni kuanza.
Wakulima hao walifahamishwa kuhusu bima za kilimo za vikundi ambazo zitawawezesha kukata bima kwa pamoja na kila mmoja kunufaika inavyostahili kwa gharama nafuu.
Elimu ya bima ya afya pia ilitolewa na wananchi ambapo walifahamishwa kuhusu uwepo wa Bima ya Afya kwa Wote unaomsaidia kila mtu kupata huduma ya afya bila kujali hali ya kifedha.
Lakini pia elimu ya bima nyingine zikiwemo bima za vyombo vya moto, bima za nyumba, bima za maisha zilizotolewa.
“Majanga tunayopata shambani ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa mfano kwa mwaka huu mvua nyingi sana zilinyesha na kusababisha hasara kwa wakulima ina maana tungejua mapema kuhusu elimu ya bima tungekatia bima kwa manufaa yetu ila tunashukuru kwa mafunzo hayo tutaanza kufanyia kazi” Restituta Chepe, mmoja wa mkulima aliyepata mafunzo hayo ya bima.
Meneja wa Kanda hiyo Bw. Kurenje Mbura aliishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa ushirikiano mzuri na kusisitiza kuendelea kutoa elimu ya bima kwenye mikutano mbalimbali wanayoiandaa ili elimu hiyo iweze kumfikia kila Mtanzania na kufahamu umuhimu wa bima katika kujikinga na umaskini.
TIRA Kanda ya Ziwa Tanganyika inahudumu mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA.