Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
WANAWAKE NA BIMA: ZOEZI LA BIMA ELFU MOJA LAWAFIKIA JUWAKITA
14 Sep, 2024
WANAWAKE NA BIMA: ZOEZI LA BIMA ELFU MOJA LAWAFIKIA JUWAKITA

ZOEZI LA BIMA ELFU MOJA LAWAFIKIA JUWAKITA

Leo Septemba 14, 2024 Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) wamepatiwa elimu ya bima kupitia shughuli maalum iliyoandaliwa na wanawake hao katika Mkoa wa Geita wakiongozwa na viongozi wao wakiwemo Mwenyekiti wa JUWAKITA Taifa, Mama Shamim Khan na Mwenyekiti Jumuiya hiyo Mkoa wa Geita, Mama Zaituni Hussein pamoja na wajumbe wengine. 

Elimu hiyo imetolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ikiwakilishwa kwenye tukio hilo na Bw. Ayubu Mremi, Afisa Takwimu Bima na Bw. Abubakari Kafumba, Afisa Uhusiano kwa Umma ambapo lengo kuu lilikua ni kuwafikishia elimu ya bima akina mama hao ili wapate uelewa wa masuala ya bima na umuhimu wake ili kupata uhakika wa matibabu pindi magonjwa yanapoibuka pasipo kutarajiwa. Zoezi hii ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zuber ya kutoa bima za afya kwa watanzania ambapo katika awamu hii ya kwanza zitatolewa bima elfu moja bure.

Jumuiya hiyo inawakilisha kundi kubwa la akina mama walio na wasio waislamu kwenye jamii zetu wakiwa ndio walezi wakuu kwenye ngazi ya familia. Katika misingi ya malezi bora miongoni mwa jamii zetu, ni dhahiri kuwa mama akiwa kama mlezi wa familia ndio anayesimamia kuhakikisha si tu familia zinapata malezi bora bali pia wanachangia kuhakikisha kaya zinakuwa na ustawi wa afya njema hasa kujikinga na maradhi na kupata matibabu inapotokea mmoja ameugua.

Hivyo, elimu hiyo ya bima waliyopata wanawake hao itawajenga kuwa mabalozi bora sio tu kwenye ngazi ya familia lakini pia kuwahamasisha makundi mengine katika jamii kutumia fursa kama hii kuhakikisha wanakua mstari wa mbele katika kukuza jamii zenye muamko wa kujikinga na kukabiliana na madhara ya majanga au changamoto zisizotarajiwa za kiafya pindi inapohitajika kupata matibabu. 

Mwenyekiti wa JUWAKITA, Mama Shamim Khan amewasisitiza akina mama hao kuchangamkia fursa hio kwa kujiandikisha ili kupata bima hizo za afya kwa ustawi wa afya ya familia zao na jamii kwa ujumla. Kwa kuwa mama ndio mlezi mkuu ni rahisi kuchangia katika kufanya maamuzi sahihi ili kulinda afya za wanafamilia wanapohitaji kupata matibabu. Amesema,” Tayari bima imefika milangoni kwenu, wote tumeona faida ya bima, msilaze damu wala msikate tamaa. Ombi langu kwenu akina mama nendeni mkajiandikishe kwakuwa bima hizi zinazotolewa ni bure, changamkieni fursa hii”.

Katika kuhakikisha elimu hiyo ya bima inawafikia vena akina mama hao, Bw. Ayubu Mremi amesema,”Ni dhahiri kuwa wanawake kuwa akina mama kunawapa sehemu kubwa katika malezi kwenye jamii zetu. Bima hizi elfu moja zitakazotolewa ni bure kabisa, hivyo wewe na familia yako mtaweza kupata huduma za matibabu bila kuingia gharama yoyote kwa mwaka mzima. Hii itasaidia kuondoa changamoto ya kukosa matibabu kutokana na ukosefu wa fedha”.

Kupitia zoezi hili la utoaji elimu ya bima elfu moja, ni wazi kuwa TIRA imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha akina mama, kama nguzo muhimu za familia, wanapata uelewa juu ya umuhimu wa bima ya afya. Elimu waliyoipata itawawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko ndani ya familia zao na jamii kwa ujumla. Wito wa viongozi wa JUWAKITA unasisitiza kuwa akina mama wachangamkie fursa hii ya bima bure ili kuhakikisha ustawi wa afya za familia zao. TIRA inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwafikia wananchi wote na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya kupitia huduma za bima. Hili ni jambo la kupongezwa na linatoa mwamko na hamasa ya kuweka afya mbele kwa kila familia.