WATANZANIA 10,000 WENYE UHITAJI KUNUFAIKA NA HUDUMA YA BIMA YA AFYA KUTOKA TIRA
Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware ameahidi kuwakatia Bima Watanzania 10,000 wenye uhitaji.
Hayo yamelezwa Julai 5, 2024 Jijini Dar es Salaam na Bi. Hawa Mniga Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) wakati akimuwakilisha Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo A. Saqware kwenye hafla fupi ya Uzinduzi wa Kitabu cha Maadili kwenye Ukumbi wa Ofisi za Bakwata.
Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba Kamishna wa Bima ameahidi kutoa sadaka ya Vitambulisho vya Bima ya Afya kwa Watanzania elfu kumi wenye uhitaji ikiwa ni juhudi za kuunga mkono serikali katika kuhakikisha Afya za Watanzania zinaimarishwa kwa kulindwa na bima.
Aidha ameongeza kusema kuwa Wananchi wote wanapaswa kukata bima kwa kuwa ni muhimu ili kuweza kujikinga na majanga mbalimbali na kwa kuwa sasa kuna bima ya Takaful inayofuata sharia na misingi ya dini ya Kiislam.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zuberi Ally ameishukuru TIRA kupitia kwa Kamishna kwa msaada huo wa bima za afya kwa Watanzania elfu kumi.
Akizungumzia kuhusu kitabu chake amesema kitabu hicho chenye jina “Mmomonyoko wa Maadili “Nani alaumiwe”? kinaeleza mambo mbalimbali yanayohusu mmomonyoko wa maadili, mitandao ya Kijamii, ukatili wa kijinsia, Kupotea kwa maadili na madawa ya kulevya.
TIRA kwa soko salama la bima.