Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
WATOA HUDUMA BIMA KANDA YA KASKAZINI WATAKIWA KUTOA ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI KUHUSU MASWALA YA BIMA .
10 Oct, 2024
WATOA HUDUMA BIMA KANDA YA KASKAZINI WATAKIWA KUTOA ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI KUHUSU MASWALA YA BIMA .

WATOA HUDUMA BIMA KANDA YA KASKAZINI WATAKIWA KUTOA ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI KUHUSU MASWALA YA BIMA .

Arusha.Watoa huduma za bima kanda ya kaskazini wametakiwa kutoa elimu zaidi juu ya maswala ya bima kwa wananchi wanaowahudumia kwani wengi wao hawana uelewa wa kutosha kuhusu maswala hayo.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TIRA kanda ya kaskazini, Bahati Ogolla wakati akizungumza katika kikao kazi  kilichowashirikisha watoa huduma wa bima kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Tanga) mnamo tarehe 25 Septemba, 2024.

Amesema lengo la kikao hicho ni kukutana na wadau hao na kuweza kujadili changamoto zinazowakabili , kuzitafutia suluhu ili kukuza soko la bima.

Aidha, Bw. Ogolla   amewataka kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu hiyo katika Makundi mbalimbali nchini ili kufikia shabaha ya 80% kwa mwaka 2030 ya watanzania kuwa na uelewa wa bima na bidhaa zake .

"Nawaombeni sana muongeze  bidii katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya bima kwani elimu bado haijatolewa vya kutosha na mpite pia  katika Makundi ambayo hayajafikiwa vya kutosha ikiwemo migodini na vijijini ambapo bado wananchi wengi wana uhitaji wa bidhaa za bima na elimu ya bima" amesema Ogolla.


Aidha amewataka watoa huduma wote kutekeleza makubaliano yote  yaliyotolewa katika kikao kazi hicho  na kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kupata mrejesho .


Ameongeza kuwa ,TIRA ni taasisi ya serikali iliyoundwa chini ya sheria ya bima Na.10 ya mwaka 2009 (sura ya 394), taasisi hii iko chini ya Wizara ya Fedha  ikiongozwa na Kamishna wa Bima  ambapo majukumu yake makubwa ni kusimamia soko la bima na kulinda haki za wateja/walaji wa bima.


Kwa upande wake Afisa leseni na usajili kutoka LATRA, Bw. John Joseph amesema kuwa,kitendo cha TIRA kuwakutanisha wadau hao kinasaidia  sana katika kujadili kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazowakabili sekta ya bima na kuweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka. 

Hata hivyo, amewataka wadau kuhakikisha wanakata bima sahihi kulingana na miongozo iliyotolewa na Mamlaka ili kuondokana  na changamoto mbalimbali zinazoweza  kutokea. 

Naye Meneja masoko kutoka kampuni ya bima ya Bumaco mkoani Kilimanjaro, Gasto Mrema amesema kuwa, kupitia kikao hicho wameweza kuelezea changamoto mbalimbali  zinazowakabili na kuweza kutoa maoni ya pamoja namna ya kuweza kupata ufumbuzi wa haraka utakaosaidia katika soko la bima .

Amesema kuwa, wamekuwa wakipeleka elimu kwa jamii  ikiwa ni pamoja na kutafuta aina mpya ya soko ili kuhakikisha majanga hayatokei tena .

"Sisi tumekuwa tukitoa  mikataba ya muda mfupi na mrefu  ,pamoja na kutoa elimu kuhusu uwekezaji, bima ya majengo ,uwekezaji kwenye SACCOS ambapo tupo nchi nzima katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka na karibu pale inapohitajika na tumekuwa tukifanya vizuri sana na kutoa elimu kila mahali ."amesema Mrema .