Uteuzi wa Bw. Frank Fred Shangali kuwa Meneja Usimamizi wa Kampuni ya Bima ya IGT
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, amemteua Bw. Frank Fred Shangali wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuwa Meneja Usimamizi wa Kampuni ya Bima ya Insurance Group of
Tanzania (IGT), kuanzia tarehe 19 Julai, 2024. Uteuzi huo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 165 (1) (iv) cha
Sheria ya Bima Sura 394 ambacho kinampa Mamlaka Kamishna kuteua Meneja wa muda ambaye atakuwa
msimamizi wa Kampuni ili kuimarisha utendaji wa Kampuni husika.
Uteuzi wa Bw. Shangali ni moja ya hatua ambazo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imechukua ili
kuboresha shughuli za kiutendaji za kampuni ya IGT na kwamba mabadiliko hayo pamoja na mengine
yanalenga kuimarisha utendaji wa Kampuni ili iweze kuendelea kutoa huduma bora za kibima kwa
wananchi kama inavyotarajiwa na Mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Bima.
TIRA itaendelea kuwa bega kwa bega na kampuni za Bima nchini ili kuhakikisha soko la bima linaendelea
kuwa salama, himilivu, lenye weledi na wakati wote itaendelea kulinda na kusimamia haki za Mteja wa
Bima.