Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wataalamu wa Uchunguzi na Udanganyifu katika masuala ya bima
09 May, 2025
Uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wataalamu wa Uchunguzi na Udanganyifu katika masuala ya bima

Jumuiya ya Wataalamu wa Uchunguzi na Udanganyifu katika masual ya Bima  (IASIU) ni jumuiya ya kimataifa inayopambana  na udanganyifu wa bima kupitia elimu, mafunzo, na ushirikiano kati ya wataalamu wa sekta ya bima, vyombo vya utekelezaji wa sheria, na mamlaka za udhibiti. Tawi la Tanzania la IASIU limeanzishwa hivi karibuni ili kushughulikia masuala ya udanganyifu wa bima yanayohusiana na mazingira ya Tanzania.

Kuanzia tarehe 14 hadi 16 Mei 2025, IASIU Tanzania itafanya Uzinduzi na Mkutano wake wa Kila Mwaka katika Jengo la PAPU, Arusha. IASIU Tanzania inashirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika maandalizi ya tukio hili. Mkutano huu utajumuisha hotuba za wazungumzaji wakuu, mijadala ya paneli, warsha, na fursa za kujenga mtandao wa ushirikiano zinazolenga kuimarisha mikakati dhidi ya udanganyifu wa bima nchini Tanzania.

Mkutano huu utawaleta pamoja wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za serikali na binafsi, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wadau kutoka sekta ya bima na kifedha kwa ujumla.

Mada mbalimbali zitajadiliwa, zikiwemo: Hali na Muonekano wa Udanganyifu wa Bima Tanzania na Afrika - Mwelekeo wa sasa, vitisho vinavyoibuka na changamoto, Jukumu la Wasimamizi katika Kupambana na Udanganyifu wa Bima, Misingi ya Uchunguzi wa Udanganyifu wa Bima, Kufichua Udanganyifu wa Bima katika Sekta ya Benki, pamoja na mada nyingine za kuvutia.

Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi na viongozi wengine kama Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP. Camillus Wambura na wengine wengi.

Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware pia atakuwepo pamoja na Naibu Kamishna wa Bima Tanzania Bi. Khadija Said na viongozi wengine kutoka TIRA.