Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
“Wasanii kateni bima kwa ajili ya kinga ya afya zenu na bidhaa zenu” – Mhe. Kabudi
02 May, 2025
“Wasanii kateni bima kwa ajili ya kinga ya afya zenu na bidhaa zenu” – Mhe. Kabudi

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Palamagamba Kabudi ameyasema hayo katika hotuba yake wakati wa kufunga rasmi Maonesho ya Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa, akiwasisitiza wasanii hapa nchini kuhakikisha wanakata bima za afya na nyinginezo kwa ajili ya kuzilinda kazi zao. Mhe. Waziri ameyafunga rasmi maonesho hayo leo tarehe 30 Aprili ambayo yalianza Aprili 24, 2025, katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Awali alipotembelea banda la TIRA katika maonesho hayo alipewa maelezo na Meneja wa TIRA kanda ya Mashariki Bw. Zakaria Muyengi kuhusu majukumu ya Mamlaka na vipaumbele vyake ikiwemo usimamizi na udhibiti wa bima ya afya kwa wote, ambapo Mamlaka inasimamia na kudhibiti skimu za bima ya afya kwa kuhakikisha zinatoa huduma za bima ya afya kwa wanachama wake na vituo vya huduma ya afya vilivyoingia mkataba na skimu kufanya kazi zake kwa weledi ikiwemo kusajiliwa.

Aidha, Mhe. Kabudi pia alizipongeza taasisi za fedha zilizoshiriki ikiwemo TIRA kwa ushiriki wake na kuwatangaza kuwa wadau wa kudumu wa Maonesho hayo ambayo yatafanyika tena mwaka 2026, Octoba jijini Arusha.

Naye,Bi.Nyakaho Mturi Mahemba, Afisa Mtendaji Mkuu kutoka Mfuko wa Utamaduni Tanzania ambao ndio waandaaji Maonesho hayo aliwasisitiza wasanii hasa vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika maonesho hayo kutoka katika taasisi za Serikali na binafsi kupitia bima, uwekezaji na nyinginezo ili waweze kunufaika katika kazi zao. 

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA